Jumanne, 15 Agosti 2017

MANISPAA YA UBUNGO YAZINDUA MAGARI MATANO(5) ( Pick up - HILUX) MAPYA KWA AJILI YA UKUSANYAJI WA MAPATO.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg. John Lipesi Kayombo (kushoto), Afisa utumishi mkuu wa Manispaa hiyo Ndg. Ally J. Ally na Mweka hazina wa Manispaa Ndg. Jane Machicho wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari matano mapya aina ya Pick - up HILUX.
Leo Jumanne August 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inayoongozwa na Mkurugenzi Ndg. John Lipesi Kayombo imezindua magari matano mapya Aina ya Pick- up Hilux waliyoyanunua kwa fedha za mapato ya ndani ( OWN SOURCE).

Ikiwa ni moja ya mikakati ya awali ya Manispaa hii katika kuboresha mapato ya ndani yatakayoleta maendeleo katika maeneo mbalimbali ya kijamii kama Hospitali, zahanati, shule na Ujenzi wa vituo vya afya magari hayo yote yamepelekwa katika idara ya Fedha na biashara kitengo Cha Mapato.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa magari hayo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg. John Lipesi Kayombo alisema ununuaji wa magari hayo ni kwa ajili ya kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa kuzipeleka Gari hizo kwa wakusanyaji wa mapato moja kwa moja ambao wako kwenye kata na mitaa ndani ya Manispaa ya ubungo.

"Manispaa ya Ubungo tulikuwa na magari machache sana, ukusanyaji wa mapato ulikuwa ni mzuri lakini tumeona bora tuongeze vitendea kazi ili kufikia lengo letu la kukusanya zaidi shillingi billioni 23 ambayo ndio Bajeti ya 2017/18 ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 100 na kuweza kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi" alisema Kayombo.

Pia Mkurugenzi Kayombo aliwashukuru Madiwani sambamba na watumishi wa Manispaa hiyo kwa ushiriki wao na hatimaye kuweza kuongeza mapato ya Manispaa hiyo.

Akizungumza baada ya uzinduzi na kukabidhiwa magari hayo kwa niaba ya Idara ya fedha mwaka hazina wa Manispaa ya Ubungo Ndg. Jane Machicho alimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na menejimenti nzima kwa kutatua changamoto ya usafiri katika ukusanyaji wa mapato kwani itasaidia kuboresha ukusanyaji wa mapato hayo na hatimaye kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato la shilingi billioni 23 kwa mwaka.

Manispaa ya Ubungo tangu kuanzishwa kwake ambapo ni takribani miezi tisa sasa imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha mapato ya manispaa ambapo moja wapo ilikuwa ni kutatua tatizo la usafiri katika ukusanyaji wa mapato katika kata za wilaya ya Ubungo.

Hongera Baraza la Madiwani, Mkurugenzi na menejimenti nzima ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

#UBUNGO YA TOFAUTI

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO-UMC

Jumatatu, 5 Juni 2017

Makamu wa Rais avitangazia hatari viwanda na migodi inayoharibu mazingira


 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa viwanda na migodi ambayo inafanya shughuli zake za uzalishaji kwa kuharibu mazingira ikiwemo utitirishaji wa kemikali kwa wananchi kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa wananchi na viumbe hai wengine.

Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo tarehe 4-Jun-2017 kijijini Butiama mkoani Mara wakati anahutubia wananchi katika kilele cha siku ya mazingira Duniani.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema uharibifu wa mazingira ukiachiwa uendee nchini ni hatari kwa usalama wa maisha na viumbe hivyo ni muhimu kwa viongozi katika ngazi zote kuchukua hatua zitakazosaidia kukabiliana na vitendo hivyo kote nchini.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa umefika wakati kwa viongozi kwa ushirikiano na jamii kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuokoa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuai, kudhibiti uchomaji miti kiholela ili kurejesha uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu katika maeneo mengi nchini.

“Kutozingatia hifadhi ya mazingira kunaweza kusababisha kuparaganyika kwa mfumo huo na kufanya maisha yetu na ya vizazi vijavyo kuwa mashakani”. Alisisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alisema katika kuadhimisha siku ya mazingira Dunia viongozi wanapaswa kuchukua hatua za kuelimisha wananchi na kuwahamasisha ili kila mtu ashiriki katika juhudi za kuwa na uchumi unaozingatia hifadhi ya mazingira.

Kuhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa nchini, Makamu wa Rais aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuruhusu wananchi kutembelea hifadhi za taifa bila kiingilio na kusema mpango huo ni mzuri na unatakiwa kufanyika kila mwaka.

Alisema kuwa mkakati huo unalenga kuhamasisha wananchi ili kuwa mahusiano rafiki na mazingira kwa kuzingatia ukweli kwamba jinsi wananchi wanapoona ndipo wanapoamini na kuelewa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Alieleza kuwa katika kuadhimisha siku hiyo inapasa jamii kutafakari mchango wa kila sekta na kila mwananchi katika uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira January Makamba alisema Serikali imeamua kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kijijini Butiama kama hatua ya kuenzi mchango mkubwa uliofanya na baba wa taifa  mwalimu Julius Nyerere katika uhifadhi wa mazingira.

Alisema baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere alifanya kwa vitendo katika kuhifadhi mazingira ambapo alianzisha msitu wake katika eneo la Butiama hivyo wananchi wote ni lazima waige mfano huo katika kulinda na kutunza mazingira.

Kwa upande wa familia na mwalimu Nyerere wameishukuru Serikali kwa kupeleka maadhimisho hayo kijijini Butiama ikiwa ni sehemu ya kuenzi na kutambua mchango wa baba wa taifa katika uhifadhi wa mazingira nchini.

Kabla ya Kuhutubia katika Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alipanda miti katika msitu wa Mwalimu Nyerere na kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya ajali ya Ndege ya Kivita ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) uliopo katika msitu wa Muhunda katika kijiji cha Butiama mkoani MARA.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Butiama – Mara
4-June-2017.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya June 5